29/09/2024
Mwenyekiti wa Taifa wa ACT-Wazalendo, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema, Chama hicho ndicho pekee kilichobeba matumaini ya Umma wa Wazanzibari, na ndiyo maana Mikutano na Vikao vivavyoendelea sasa kote Nchini, vimechukua taswira ya kutatua changamoto za wananchi wote, ikiwa ni sehemu ya Mwongozo na Ahadi yao ya 'The Brand Promise'
Mheshimiwa Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo Septemba 29, 2024 alipokutana na kufanya mazungumzo na Wazee wa Mkoa wa Kichama wa Mkoani, huko Chole Kengeja, Mkoa wa Kusni Pemba, ikiwa ni Sehemu ya kusikiliza na kutatua changamoto zao, pamoja na kubadilishana mawazo.
Amesema, Chama hicho kinaelewa kwamba Umma wa Wananchi, kwa sasa unakabiliwa na wimbi la changamoto, zikiwemo za adha na ugumu wa maisha, bali Sera za Chama hicho katu haziwezi kuwasaliti, na Viongozi wataendekelea kuwafikia mara kwa mara kwa lengo la kuzitatua na kukabiliana nazo.
"Sisi tunaelewa kwamba sasa Wananchi wameelemewa na shida na matatizo; na pia zipo hila na njama nyingi ovu za watawala za kuwatoa Wananchi katika imani kuelekea Uchaguzi wa Oktoba 2025, bali la msingi ni kusimamia dhamira ya dhati ya Chama chetu ya kuleta Ukombozi na Mamlaka Kamili ya Visiwa hivi", amesema Mheshimiwa Othman.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho upande wa Zanzibar, Ndugu Ismail Jussa amesema, "zama za kudanganyana na kuwajengea hofu Wananchi zimeisha, sasa ni muda wa uwazi, na katika yote haya CCM hawana manusura kwani msingi wa harakati hizi una mizizi mikubwa na upo nyoyoni mwetu",
Jussa amewahimiza Wazee hao kuwa dira njema kwa jamii zao, ili Vijana nao wafuate Kigezo cha kuipigania Heshima ya Nchi hii.
Kikao hicho ambacho kimefanyika katika Ukumbi wa Judo, uliopo Chole, Shehia ya Kengeja, Jimbo la Mtambile Mkoa wa Kusini Pemba, kimewajumuisha pia Wazee wa Chama, Wazee wa Mji, Watu Mashuhuri, Masheikh pamoja na Viongozi mbali mbali, wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa ACT- Wazalendo Zanzibar, Omar Ali Shehe.
Mheshimiwa Othman ambaye yupo kisiwani Pemba kwa ziara maalum inayojumuisha shughuli za Kisiasa, Serikali na kijamii, akiwa ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, jioni ya leo atahutubia Mkutano wa Hadhana katika jimbo Chambani pia Mkoa wa Kusini Pemba.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Septemba 29, 2024.