18/05/2026
CAN Tanzania tunamshukuru Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, kwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la CAN Tanzania, Dkt. Sixbert Mwanga.
Katika mazungumzo yaliyofanyika Mei 14, 2026 katika Ofisi ya Makamu wa Rais, Luthuli, jijini Dar es Salaam, zaidi ilikuwa ni namna ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa asasi za kiraia unavyoweza kufanikisha utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya nchi hususani Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Dkt. Muyungi alisisitiza kuwa Ofisi yake imefungua zaidi milango ya ushirikiano na wadau wa sekta binafsi ili kuimarisha jitihada za uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hatua ambayo itasaidia jamii na taifa kwa ujumla. Pia alieleza kuwa Serikali inatekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hivyo wadau wote wanapaswa kushirikiana kwa karibu kuweka mazingira wezeshi ya kufikia malengo hayo.
Kwa upande wake, Dkt. Sixbert Mwanga aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kuendelea kushirikiana na CAN Tanzania katika utekelezaji wa miradi na programu mbalimbali za mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza kuwa CAN Tanzania, kupitia ofisi zake za Dar es Salaam na Zanzibar, itaendelea kujikita katika uhamasishaji wa matumizi endelevu ya rasilimali, na ushirikiano wa kimkakati ili kuunga mkono vipaumbele vya maendeleo ya nchi, na jitihada za nchi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambazo zinaendana na Mpango Mkakati wa CAN Tanzania 2024–2029.